Mh.Waziri Ahitimisha Maonyesho ya Nane Nane Kitaifa


Mh.Waziri  Ahitimisha Maonyesho ya Nane Nane Kitaifa
24
August
2017

Serikali imesema kuwa imefuta baadhi ya kodi na tozo ili kuwanufaisha wakulima wote nchini ambao awali walikuwa wakilalamikia na kupinga tozo na kodi hizo kwa madai kuwa zilikuwa zikiwanyonya sio kuwakwamua na wimbi kubwa la umasikini.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba wakati alipotembelea banda la Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi wakati wa Maonesho ya Kilimo (Nanenane) yanayofanyika katika Viwanja vya Ngongo Mkoani Lindi.

Dkt Tizeba Alisema kuwa kwa muda mrefu serikali imekuwa ikipata malalamiko kutoka kwa wananchi mbalimbali hususani kwa wakulima nchini Tanzania wakipinga kodi na tozo mbalimbali zinazotozwa kwani zimekuwa zikiwanyonya badala ya kuwakwamua na wimbi kubwa la umasikini jambo ambalo serikali ililitazama na kuona umuhimu wake na hatimaye kufikia utekelezaji huo.

Ameyasema kuwa hayo ya Nanenane ambayo Kitaifa yanafanyika Mkoani Lindi yenye kauli mbiu ya “Zalisha kwa Tija Mazao na Bidhaa za Kilimo Mifugo na Uvuvi ili kufikia Uchumi wa Kati” yanayofanyika yamedhamiria zaidi katika kumkwamua mkulima kutoka kwenye kilimo kwa ajili ya mahitaji ya ndani na kufikia hatua ya kilimo biashara.

Dkt Tizeba Alisema kuwa Jumla ya tozo 80 kati ya tozo 139 zimefutwa na tozo nne (4) zimepunguzwa viwango. Tozo, kodi na ada zinajumuisha kufutwa kwa tozo kumi (10) na mbili (2) kupunguza viwango kwenye zao la tumbaku. Kwenye zao la kahawa zimefutwa tozo 17 na moja (1) kupunguzwa kiwango; sukari zimefutwa 16; pamba tozo zilizofutwa ni mbili (2); kwenye korosho tozo mbili zimefutwa na chai imefutwa tozo moja (1).

Katika kuongeza upatikanaji wa pembejeo tozo tatu (3) zimefutwa na moja (1) imepunguzwa kiwango kwenye mbolea na tozo saba (7) zilizokuwa kwenye mbegu nazo zimefutwa. Katika Ushirika jumla ya tozo 20 zimefutwa katika ngazi mbalimbali.

Katika Mifugo; kodi, ada na tozo saba (7) ambazo zilikuwa kero kwa Wafugaji, Wafanyabiashara na Wawekezaji nazo zilifutwa na kubakiza zile tu zenye uhusiano wa moja kwa moja katika uendelezaji wa Sekta ya Mifugo. Tozo zilizofutwa zinajumuisha mbili (2) kwenye maziwa; nyama tozo nne (4) na moja (1) kwenye afya ya mifugo.

Katika Uvuvi, jumla ya kodi, ada na tozo tano (5) ambazo ni kero kwa Wavuvi, Wafugaji wa viumbe kwenye maji na wawekezaji nazo zimefutwa.